1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Hatari ya uhalifu wa kivita ni kubwa Gaza

Mohammed Khelef
6 Desemba 2023

Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanaishi katika khofu kubwa, huku ukitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita kati ya Israel na Hamas.

https://p.dw.com/p/4ZqLJ
Gazastreifen Israel Krieg mit Hamas
Hali katika kiunga cha Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumatano (Disemba 6, 2023).Picha: Ahmed Zakot/REUTERS

Volker Turk amesema kuna hatari kubwa ya kufanyika uhalifu mkubwa wa kivita katika mazingira ya aina hiyo ya kiwango cha maafa makubwa ya kibinaadamu.

Mkuu huyo wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa amesema watu milioni 1.9 kati ya milioni 2.2 wanaoshi katika ukanda huo wameyakimbia makaazi yao na wanaendelea kusukumwa katika maeneo yanayozidi kupungua yenye msongamano mkubwa wa watu kusini mwa Gaza katika mazingira machafu na yasiyo bora kwa afya.

Soma zaidi: Mzozo wa Gaza hauna mithili ukiangalia vifo vya wanahabari

Hayo yanajiri wakati wanajeshi wa Israel wakiendelea kukabiliana na wanamgambo wa Hamas huko Gaza baada ya kutanua operesheni yao ya mashambulizi ya ardhini hadi mji wa pili kwa ukubwa wa Khan Younis.

Hatua hiyo inaathiri pakubwa usambazaji wa msaada muhimu katika maeneo mengi ya ukanda huo.